Daniel 10

Maono Ya Danieli Kuhusu Mtu

1 aKatika mwaka wa tatu wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, Danieli (ambaye aliitwa Belteshaza) alipewa ufunuo. Ujumbe wake ulikuwa kweli, nao ulihusu vita vikubwa. Ufahamu wa ujumbe ulimjia katika maono.

2 bWakati huo, mimi Danieli nikaomboleza kwa majuma matatu. 3 cSikula chakula kizuri; nyama wala divai havikugusa midomo yangu; nami sikujipaka mafuta kamwe mpaka majuma matatu yalipotimia.

4 dKwenye siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa nimesimama kwenye ukingo wa mto mkubwa Hidekeli,
Hedekeli ndio Mto Tigrisi.
5 fnikatazama juu, na mbele yangu alikuwepo mtu aliyevaa mavazi ya kitani na mshipi wa dhahabu safi kutoka ufazi kiunoni mwake. 6 gMwili wake ulikuwa kama kito cha zabarajadi safi, uso wake kama umeme wa radi, macho yake kama mwali wa moto, mikono yake na miguu yake kama mng’ao wa shaba iliyosuguliwa sana, nayo sauti yake kama ya umati mkubwa wa watu.

7 hMimi Danieli, ni mimi peke yangu niliyeona hayo maono; watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona, lakini waligubikwa na hofu kuu, hata wakakimbia na kujificha. 8 iKwa hiyo niliachwa peke yangu, nikikodolea macho maono hayo makubwa; sikubakiwa na nguvu, na rangi ya uso wangu ikabadilika kama aliyekufa, nikakosa nguvu. 9 jKisha nikamsikia akisema, nami nilipokuwa nikimsikiliza, nikalala kifudifudi, nikapatwa na usingizi mzito.

10 kMkono ulinigusa, ukaninyanyua, na kuniweka nikipiga magoti na mikono yangu ikashika chini, huku nikiwa bado ninatetemeka. 11Akasema, “Danieli, wewe mtu upendwaye sana, fikiri kwa makini maneno ninayokwenda kunena nawe sasa; simama wima, kwa maana sasa nimetumwa kwako.” Naye aliponiambia haya, nikasimama nikitetemeka.

12 lNdipo akaendelea kusema, “Danieli, usiogope. Tangu siku ya kwanza ulipotia moyo wako ili kupata ufahamu na kujinyenyekeza mbele ya Mungu wako, maneno yako yalisikiwa, nami nimekuja ili kujibu maneno yako. 13 mLakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga kwa siku ishirini na moja. Ndipo Mikaeli, mmoja wa malaika wakuu, alikuja kunisaidia, kwa sababu nilikuwa nimezuiliwa huko na mfalme wa Uajemi. 14 nSasa nimekuja kukuelezea mambo yatakayowatokea watu wako wakati ujao, kwa maana maono hayo yanahusu wakati ambao haujaja bado.”

15 oAlipokuwa akinielezea haya, nilisujudu uso wangu ukiwa umeelekea chini, nikawa bubu. 16 pNdipo mmoja aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa midomo yangu, nami nikafungua kinywa changu, nikaanza kunena. Nikamwambia yule aliyesimama mbele yangu, “Nimepatwa na huzuni kubwa kwa sababu ya maono haya, bwana wangu, nami nimeishiwa nguvu. 17 qBwana wangu, mimi mtumishi wako nitawezaje kuzungumza na wewe? Nguvu zangu zimeniishia hata ninashindwa kupumua.”

18 rTena yule aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa na kunitia nguvu. 19 sAkasema, “Ee mtu upendwaye sana, usiogope. Amani iwe kwako! Uwe na nguvu sasa; jipe nguvu.”

Alipozungumza nami, nilipata nguvu, nikasema, “Nena, bwana wangu, kwa kuwa umenipa nguvu.”

20 tKwa hiyo akasema, “Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa hivi nitarudi kupigana dhidi ya mkuu wa Uajemi, nami nikienda, mkuu wa Uyunani atakuja. 21 uLakini kwanza nitakuambia kile kilichoandikwa katika Kitabu cha Kweli. (Hakuna hata mmoja anayenisaidia dhidi yao isipokuwa Mikaeli, mkuu wenu.
Copyright information for SwhKC